Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza, Rais wa Jamhuri ya Burundi,
Waheshimiwa Mawaziri kutoka Burundi na Tanzania,
Mheshimiwa Issa Ntambuka, Balozi wa Burundi nchini Tanzania,
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Burundi na Tanzania waliopo,
Makatibu Wakuu na Watendaji mbalimbali wa Serikali za nchi zetu mbili,
Ndugu wananchi, Mabibi na Mabwana,
Shukrani
Ni furaha kubwa sana kwangu kukukaribisha Tanzania Mheshimiwa Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi na ujumbe wako kwa ajili ya shughuli hii muhimu na ya kihistoria katika uhusiano wa nchi zetu mbili. Wewe na mimi kuwepo Mugikomero kuzindua zoezi la uwekaji wa mawe ya mpaka baina ya Burundi na Tanzania ni kielelezo tosha cha uhusiano mwema, udugu na urafiki uliopo kati ya nchi zetu mbili na watu wake.
Uhusiano wa Tanzania Burundi
Kama sote tujuavyo nchi zetu tatu za Burundi, Rwanda na Tanganyika sasa Tanzania Bara, kabla ya Vita Kuu ya Kwanza tulikuwa nchi moja chini ya utawala wa Wajerumani na kujulikana kama German East Africa. Ni baada ya Vita Kuu hiyo na Wajerumani kushindwa ndipo tukawa nchi tatu yaani Tanganyika chini ya utawala wa Waingereza na Burundi na Rwanda zikiwa nchi mbili chini ya Wabelgiji.
Umuhimu wa Kuhakiki Mpaka
Ndugu Wananchi,
Mnamo tarehe 5 Agosti 1924, ndipo Mkataba wa Mpaka wa nchi zetu hizi mbili, ulipotiwa saini. Leo miaka 90 baadae tupo kwenye mchakato wa kuhakiki mpaka wetu. Zoezi hili litapelekea nchi zetu kuwa na Mkataba mpya wa Mpaka ambao sasa utakuwa ni wetu wenyewe. Kama zilivyo nchi nyingi za Kiafrika, Tanzania na Burundi zilirithi mpaka uliopo kutoka kwa waliokuwa watawala wetu enzi za ukoloni. Mpaka huu haujafanyiwa mapitio wala kuimarishwa tangu nchi zetu zipate uhuru zaidi ya miaka 50 iliyopita. Katika kipindi hicho kumekuwepo na mabadiliko mbalimbali ikiwemo ongezeko la watu na shughuli za kiuchumi na kimaendeleo katika maeneo ya mipakani. Aidha katika baadhi ya maeneo hata alama za mipaka zimekuwa vigumu kuzitambua ama kwa sababu ya kuchakaa au mawe kung’olewa. Hali hiyo haiwezi kuachwa kuendelea ilivyo.
Kwa kutambua ukweli kwamba kwa baadhi ya nchi utata kuhusu mipaka kuwa kiini cha migogoro, Kikao cha Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika (AU) kilichofanyika Accra, Ghana tarehe 27 Juni, 2007 kilizitaka Nchi zote Wanachama wa Umoja wa Afrika kushirikiana katika kuimarisha mipaka yao ifikapo mwaka 2012. Hata hivyo, kipindi hicho kiliongezwa hadi kufikia mwaka 2017. Tumebaki na miaka mitatu kabla ya muda huo kukamilika, hivyo tunafanya zoezi hili ndani ya wakati wake.
Zoezi za Kuimarisha Mpaka
Ndugu Wananchi,
Nchi zetu ziliitikia wito huo wa Umoja wa Afrika (AU) kwa kuunda Kamati ya Pamoja ya Wataalamu ambayo ilikagua mpaka mzima na kubaini mawe yaliyong’olewa, mawe yaliyoharibiwa na kuainisha maeneo ambayo yalikuwa yanastahili kuongezewa mawe ili yaweze kuonekana vizuri miongoni mwa wananchi waishio mpakani.
Zoezi hili ni kubwa na lina changamoto zake. Mpaka wa Tanzania na Burundi una urefu wa Kilometa 450 ambao ni sawa na umbali wa kutoka Dar es Salaam hadi Lindi. Isitoshe mpaka hauko mijini, maeneo mengi yako misituni kwenye mabonde na milima. Ni magumu kuyafikia. Kwa upande wetu mpaka upo katika mikoa miwili ya Kagera na Kigoma na kwenye wilaya tano, kati ya hizo nne ni za Mkoa wa Kigoma (Kigoma, Kasulu, Kibondo na Kakonko) na moja ni hii ya Ngara iliyoko mkoa wa Kagera. Aidha, zoezi hili lina gharama kubwa na hatuna mfadhili hivyo linagharamiwa na nchi zetu mbili. Hali yetu tunaijua lakini tumeamua kufanya wenyewe jambo linaloonyesha utashi mkubwa wa Serikali zetu mbili katika kufanikisha zoezi hili muhimu sana.
Wito kwa Wananchi Waishio Mpakani
Ndugu Wananchi,
Lengo la zoezi hili sio kuwatenganisha wakazi wa mpakani ambao sote tunatambua kwamba shughuli zenu zinaingiliana na wengine mna uhusiano wa kifamilia na kidugu. Tunachokifanya leo ni kuimarisha mpaka na kuwatengenezea mazingira yenu kuwa mazuri zaidi. Kurasimisha mipaka kunafanya kazi za kiutawala mpakani kuwa rahisi baina ya mamlaka za pande zote mbili za mpaka. Kunaweka taratibu nzuri za kurasimisha utoaji wa huduma za umma na kuwezesha maingiliano ya kidugu na kibiashara baina ya watu wa Burundi na Tanzania. Hivyo, kitendo cha kuweka mambo sawa na sio kuwakwaza.
Ndugu wananchi,
Mpaka huu ni wenu. Nawaomba muwe walinzi wa mawe tutakayoweka leo na siku za usoni. Tusiyang’oe au kuyaharibu. Hakuna sababu ya kufanya yote hayo. Maana naambiwa hata baadhi ya sababu hazina maana tena na za kipuuzi. Kwa mfano, ipo dhana potofu kwamba kuna mali za thamani zilizofichwa kwenye mawe hayo. Nafurahi kwamba baadhi ya vijana wenu wanashirikishwa kwenye zoezi hili. Hivyo wao ndiyo mashahidi kwamba mawe haya ni mchanganyiko wa sementi, kokoto na mchanga. Hakuna dhahabu wala vito vingine vya thamani kama ambavyo ilivyokuwa ikidhaniwa miaka ya nyuma na hivyo kupelekea mawe zaidi ya sita kung’olewa. Sisi tuwe ni kizazi cha mwisho kuhujumu mawe ya mpakani kwa sababu yo yote ile. Lazima tutambue kwamba ni jambo baya kufanya hivyo na kwamba ni kujihujumu wenyewe kwani ujenzi wa kurudishia mawe yaliyong’olewa utagharamiwa kwa fedha ambazo zingefanya jambo linguine la manufaa.
Pongezi
Ndugu Wananchi,
Napenda kutumia fursa hii kuipongeza Kamati ya Wataalamu kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya mpaka tumefikia kuwa na hafla hii ya leo ya kihistoria. Wamefanya kazi yao kwa bidii, uaminifu, uadilifu na weledi wa hali ya juu. Wamejali na kuzingatia maslahi ya nchi zetu. Ni wazalendo wa dhati. Daima majina yao yatakuwemo kwenye vitabu vya kumbukumbu na historia ya nchi za Tanzania na Burundi.
Hatma
Baada ya kukamilisha zoezi la kuweka mawe ya Mpaka mzima, utaandaliwa Mkataba wa Mpaka baina ya Nchi zetu ambao utafuta ule wa Kikoloni wa Mwaka 1924. Ni matumaini yangu kwamba wataalamu wetu wataongeza kasi ili zoezi hili likamilike mapema. Kwa ajili hiyo, naziagiza Mamlaka zinazohusika kwa upande wa Tanzania kutimiza wajibu wake ipasavyo ili zisiwe sababu ya kuchelewesha au kukwamisha zoezi hili.
Ndugu wananchi;
Pamoja na zoezi hili linaloendelea, napenda kuwaarifu kuwa tunaendelea na uhakiki wa mipaka yetu na nchi za Msumbiji (kilometa 756), Zambia (kilometa 338), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (kilometa 473) na Kenya (kilometa 769). Baadae, tunakusudia, kufanya hivyo kwa mipaka yetu na Rwanda (kilometa 217), Uganda (kilometa 396) na Malawi (kilometa 475). Nazitaka Mamlaka zinazohusika kuhakikisha kuwa zoezi la kuhakiki Mipaka yote baina ya Tanzania na nchi tunazopakana nazo linafanyika kwa ukamilifu na ufanisi wa hali ya juu.
Hitimisho
Mheshimiwa Rais,
Ndugu Wananchi,
Marafiki huchora mipaka kwa mazungumzo na kalamu, maadui huichora kwa nguvu na kwa wino wa damu za binadamu. Mipaka ya kalamu hudumu kuliko ile itengenezwayo kwa damu. Mipaka ya kalamu hustawisha jamii wakati ile ya damu hufarakanisha, huzua chuki, hujuma na visasi. Kadri tunavyohakiki mipaka yetu kwa njia ya mazungumzo na kalamu, tunaondoa sababu na uwezekano wa nchi kugombana, kufarakana na hata kupigana kwa sababu ya mipaka. Sisi na Burundi ni ndugu, tumechagua njia ya mazungumzo na kalamu. Ni uamuzi sahihi, makini na wa busara na hekima kubwa. Tuzidi kumuomba Mungu atujalie na kutuongoza iwe hivyo kwa nchi zote tunazopakana nazo.
Ndugu wananchi,
Naomba nimalizie kwa kusisitiza mambo makuu matatu;
Mwisho, nakushukuru tena Mheshimiwa Rais kwa upendo na ushirikiano wako. Wewe Mheshimiwa Rais, Serikali na watu wa Burundi ni rafiki wa kweli na ndugu wa Tanzania. Nami nakuhakikishia hapatakuwa na upungufu wa ushirikiano kwa upande wangu na wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Karibu sana.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza!
Jakaya Mrisho Kikwete is a Tanzanian politician who served as the fourth President of Tanzania from 2005 to 2015. Known for his efforts in improving education, healthcare, and infrastructure, he remains an influential figure in African politics. Read Full Biography